Oktay amsifia Onyango
Kocha wa klabu ya Gor Mahia Hassan Oktay amemsifia mshambulizi Samwel Onyango baada ya kufunga mabao mawili dhidi ya timu ya Nigeria Lobi Stars kwenye mechi ya vilabu bingwa barani Africa siku ya Jumapili.
Onyango, ambaye ni mchezaji wa zamani wa klabu ya jeshi, Ulinzi Stars alifunga bao la pili na la tatu baada ya Jacques Tuyisenge kufungua ukurasa wa mabao.
Kwenye mahojiano baada ya mechi, Oktal alimsifia nyota huyo akisema kuwa ana uwezo wa kuimarika zaidi kimchezo.
“Onyango ni mchezaji mwenye kipaji kikubwa. Leo alionyesha mchezo mzuri sana na akaweza kutufungia mabao mawili. Nina imani kuwa ataimarika zaidi, uwezo anao na mimi kama kocha nitamsaidia kuwa bora zaidi,” alisema Oktay
Kocha huyo ambaye alijiunga na Gor Mahia hivi majuzi hakuridhishwa na matokeo licha ya kushinda akisema timu yake ilifaa kufunga mabao zaidi.
“Siwezi sema nimefurahishwa na matokeo kwa kuwa tulikuwa na nafasi nyingi ya kuzidisha uongozi wetu. Tungeshinda mechi hiyo kwa mabao manne au matano, kipindi cha pili ilibidi tuweze kuzuia zaidi kwani Labi Stars walimiliki mpira. Kwenye mechi ya marudiano itabidi tuweke bidii zaidi,” aliongezea raia huyo wa Uturuki.
Mechi ya marudiano itachezwa siku wikendi ijayo nchini Nigeria.