Southampton wakatisha rekodi ya Arsenal
Watakatifu Southampton wametumia utakatifu wao kuwatuliza washika bunduki wa jiji la London katika uwanja wa St.Mary.
Southampton wamemamaliza mbio za Arsenal za kutopoteza mechi 22 mfululizo baada ya kuwagaragaza kwa goli 3-2.
“ Ilibidi nikimbie kwa watu wangu kwa sababu walikuwa wananisubiri. Ndicho nilikuwa ninataka nijisikie nilivyokuja katika Premier League , hii hali baada ya mechi , na kushangilia wakati huu ni kitu kizuri sana kwangu mimi “ alisema kocha wa Southampton Ralph Hasenhuttl aliyejiunga na timu hiyo mwanzoni mwa mwezi huu akichukua nafasi ya Mark Hughes.
Danny Ings ndiye alikuwa wa kwanza kucheza na nyavu katika dakika ya 20 kabla ya kiungo wa Arsenal Henrikh Mkhitaryan dakika ya 28 kusawazisha baada ya kazi nzuri ya Alex Iwobi na Nacho Monreal.
Pasi nzuri kutoka kwa Nathan Redmond ilimkuta Danny Ings na kuuweka mpira ndani ya goli dakika moja kabla ya mapumziko.
Arsenal katika kipindi cha pili walirejea tena katika mchezo, kwa mara nyingine Henrikh Mkhitaryan anamjibu Danny Ings, na kufanya matokeo kuwa 2-2 katika dakika ya 53.
Shukurani zinaenda kwa Charlie Austin ambaye ndiye aliyeleta ushindi wa kwanza wa nyumbani katika ligi kwa Southampton tangu mwezi April, akifunga kwa kichwa kunako dakika ya 85 ya mchezo.
Kipigo hiki kwa Arsenal kinawafanya kuwa katika nafasi ya 5 huku wakipitwa pointi tatu na Chelsea ambao wapo nafasi ya nne baada ya ushindi wao wa ugenini dhidi ya Brighton.